CHUO KIKUU CHA DODOMA MWENYEJI WA MASHINDANO YA SHERIA YA UTU ( HUMANITARIAN LAW)


  • 1 year
  • School of Law

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Mashindano ya Sheria za Utu wakati wa Vita (International Humanitarian Law) yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma
Tanzania. Chuo kikuu Cha Dodoma kimefanikiwa kuwa Chuo Cha Kwanza kuchaguliwa na Shirika la Kimataifa la International Committee of Red Cross (ICRC) kuwa sehemu ambapo mashindano ya sheria za utu wakati wa vita yatafanyika.

Mashindano hayo yameanza tarehe 27 Julai na yatahitimishwa tarehe 28 Julai, 2023. Chuo Kikuu Cha Dodoma kimepewa heshima hiyo baada ya kushinda mashindano hayo Mara tatu mfululizo toka mwaka 2019, huku mwaka jana 2022 wakifanikiwa kuwa Chuo Cha Kwanza kutoka Tanzania kushinda mashindano hayo kwa Vyuo vya Afrika.

Mashindano haya yamefunguliwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof Razack Lokina ambaye alimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka. Akitoa salamu za Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lokina aliwapongeza Shule Kuu ya Sheria kwa kuweza kukiletea heshima Chuo Kikuu Cha Dodoma kupitia ushindi wa miaka mitatu mfululizo ngazi ya kitaifa. Prof. Razack pia alitoa shukrani na pongezi kwa Shirika la ICRC kwa kuwa mstari wa mbele katika kueneza elimu ya sheria za utu wakati wa vita na hasahasa kuyaleta mashindano haya UDOM.

Naye Afisa wa Sheria kutoka Shirika la ICRC ofisi za Nairobi, Kenya, Bi Jemma Arman, alisema uwepo wao UDOM utafungua mianya zaidi ya kushirikiana na UDOM katika masuala ya kitaaluma na tafiti.

Mashindano hayo yanahusisha vyuo nane kutoka Tanzania vikiwemo Chuo Kikuu Cha Dodoma, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Cha Tumaini (Dar), Chuo Cha SAUT (Mwanza), Chuo Cha SAUT (Arusha), Chuo Kikuu Cha Iringa, Chuo Kikuu Cha RUCU na Chuo Kikuu Cha Kiislam Morogoro.

Kwa tarehe 27 mashindano hayo yameanza katika hatua ya awali huku tarehe 28 mashindano hayo yakitarajiwa kuingia ngazi ya nusu fainali na fainali.

Comments
Send a Comment