DPP AWANOA WANAFUNZI WA SHERIA UDOM
Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) Bw. Sylvester A. Mwakitalu, amewaasa wanafunzi wanaosoma Sheria Chuo Kikuu Cha Dodoma kupinga vikali vitendo vya rushwa wakati wa utoaji haki hasa katika kipindi hiki ambacho dunia ipo katika matumizi makubwa ya Sayansi na Teknolojia.
Hayo ameyasema tarehe 19 Aprili, 2024 alipokutana na wanafunzi wa Sheria wa UDOM mwaka wa 3 na wa 4 katika ukumbi wa “Theatre 1” uliopo Shule Kuu ya Sheria chuoni hapo katika mhadhara uliondaliwa mahususi kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi katika masuala mazima ya kiutendaji katika utoaji haki pamoja na changamoto zilizopo katika sekta ya sharia na utoaji haki.
“Najua baada ya muda mfupi wengi wenu mtakuwa wanasheria Serikalini au katika Taasisi binafsi, ni lazima muhakikishe mnazingatia mambo makubwa matatu ambayo ni; nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kuzingatia maslahi mapana ya Umma” Alisema Bw. Mwakitalu.
Aidha, amewataka wanafunzi hao kuendelea kusoma kwa bidii hata baada ya kumaliza masomo yao kwa kuwa mambo yanabadilika kila siku. Alieleza changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa sasa kuwa ni pamoja na rushwa, vitisho kutoka kwa watuhumiwa, imani za kishirikina pamoja na mashahidi kutoroka wakati kesi zinaendelea.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Bw. Ng’ombe Masunga ambaye ni mwanafunzi wa sheria mwaka wa 4, amemshukuru DPP kwa kutenga muda wa kukutana nao na kuwashirikisha uzoefu wake mkubwa katika sekta ya sheria. Vilevile ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kumwalika mkurugenzi huyo Chuoni kwani uzoefu wake katika sekta ya sheria umewajengea uelewa mkubwa wa namna kada ya sheria inavyofanya kazi.
Kabla ya kushiriki Mhadhara huo, DPP alikutana na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Razack Lokina, ambaye amemhakikisha chuo kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kuendelea kuwatumia wataalamu wabobevu kutoka ofisi yake ili kuwajengea uwezo wanafunzi wa Sheria, ili kuendelea kuzalisha wataalamu wabobevu katika tasnia hiyo nchini.