WATAALAMU WAASWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUSUKUMA MBELE MAENDELEO


  • 8 months
  • College of Informatics and Virtual Education

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka , ameshauri Teknolojia zote zinazogunduliwa ziwe zinauwezo wa kuendelezwa kwa maendeleo ya Taifa.

Prof. Kusiluka ameyasema hayo tarehe 21 Julai, 2023 wakati wa kukagua utekelezaji wa mafunzo ya wiki mbili yanayoratibiwa na Maabara ya Utafiti wa Akili Bandia kwa Maendeleo (AI4D Research Lab) ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watalaamu mbalimbali katika matumizi ya Akili Bandia ( Artificial Intelligence) ikihusisha wafanyakazi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Sekta binafsi na Umma, pamoja na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu ikiwemo UDOM, MUST, UDSM, DIT, CBE, KIU, na NM-AIST.

"Nyinyi wenzetu ambao mmepata fursa ya kukaa hapa na kujifunza haya mambo mema mjifunze mkitanguliza mbele uzalendo kwa Taifa katika kizitumia hizi Teknolojia kwa maendeleo mapana ya nchi yetu" alisema Prof. Kusiluka

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo- Taaluma, Utafiti na Ushauri Prof. Razack Lokina, ameipongeza Ndaki ya Sayansi za Komputya na Elimu Angavu kwa kuweza kufanikisha mradi huu ambao NM-AIST ni mshirika mmojawapo.

Mradi wa Akili Bandia kwa Maendeleo ( Artificial Intelligence for Development) unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Dodoma kwa Kushirikiana na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela- Arusha. Mradi huu ni wa miaka mitatu na unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Canada (IDRC) na Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida).

Kwa upande mwingine, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu Dkt. Florence Rashid, amesema baada ya mafunzo anategemea washiriki watakuwa wamepata maarifa ambayo yatawasadia kutengeneza mifumo mbalimbali kwenye mambo ya afya, kilimo, uchumi wa kidijitali na mengineyo ambayo Akili Bandia inaweza kusaidia.

Aidha, Mtafiti mkuu wa mradi, Dkt. Ally S. Nyamawe, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni ya awamu ya pili baada ya yale yaliyofanyika mwezi Julai mwaka 2022. Amesema Lengo la mafunzo ya namna hii ni kuwaandaa wataalamu wa ndani kushiriki kikamilifu katika ushindani wa kibunifu katika kutengeneza programu za kompyuta zinazotumia teknolojia ya Akili Bandia ili kutatua matatizo yanayoikabili jamii.

Comments
Send a Comment