UDOM YAENZI TAMADUNI ZA MAKABILA YA KITANZANIA
Chuo Kiku cha Dodoma ( UDOM) kupitia Ndaki ya Sayansi ya Insia na Sayansi za Jamii ( CHSS) Idara ya Historia na Akiolojia ( DOHA) Siku ya leo tarehe 23 Mei 2025 katika Ukumbi wa Chimwaga Kimeenzi Mila na Tamaduni za Makabila 6 ya Kitanzania ( Wagogo, Wahaya, Wasukuma, Wamasai, Wahehe na Wapemba) Lengo likiwa ni kuhimiza, kuendeleza, kudumisha pamoja na kuziishi tamaduni za Kitanzania ambazo zimeonekana kupotea kutokana na mwingiliano wa tamaduni za nje na makabila.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Maonesho hayo; Mgeni Rasmi ambaye nj Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Wizara ya Maliaasili na Utalii, Dkt. Christowaja Ntandu, alisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kuwajibika kukuza na kulinda Utamaduni wake huku akitoa wito kwa vijana wa Kitanzania kuendelea kujifunza na kuvaa Utamaduni kutokana na mwingiliano wa zama za Utandawazi
"Tusione aibu, tuthamini vitu vyetu kile ambacho umesomea kifanye vilivyo"
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina, amewapongeza wanafunzi wa Mwaka wa Tatu wanaosoma somo la Ujasiriamali katika Rasilimali za Urithi wa Utamaduni ambao wameonesha kazi mbalimbali za kiubunifu ikiwemo mavazi na vyakula
" Kupitia maonesho haya tumeona jinsi elimu inavyoweza kutafsiriwa kwa vitendo, tumeshuhudia ubunifu, tunu za Utamaduni na vipaji vya wanafunzi hii inadhihirisha kuwa vijana wetu wakielekezwa vizuri wanaweza kuwa chachu ya Maendeleo nchini" Aliongeza Prof. Lokina.
Kwa upande wake; Kaimu Rasi wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii, Dkt. Zuhura Badru, amesema maonesho hayo yanaonesha mwanga namna gani elimu inaweza kutumika kama nyenzo ya kulinda Urithi wa Utamaduni lakini pia kukuza ajira kwa vijana na kuchochea utalii wa ndani.
Naye; Kiongozi wa Jadi kutoka Kabila la Wagogo Chifu Henrich Mazengo, amefurahia maonesho hayo huku akisisitiza kuwa shughuli kama hizo ziendelee zaidi ili kuikumbusha jamii umuhimu wa kuenzi na kukuza tamaduni za Kitanzania.
Maonesho hayo yameongozwa na Kauli mbiu isemayo "Utamaduni wa Tanzania ni Moyo wa Taifa, Tuulinde na Kuuenzii"