UDOM YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA MAONESHO YA NANENANE 2023
Chuo Kikuu cha Dodoma kimeibuka mshindi wa Kwanza Taasisi za Elimu ya Juu katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati katika Viwanja vya vya Nzuguni Dodoma.
Mgeni Rasmi katika Maonesho hayo Mhe. Protabas Katambi (Mb) Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) alikipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuja na bunifu ambazo zimesaidia katika kuongeza thamani katika kilimo na ufugaji kwa kutumia Teknolojia ya kisasa.
Moja ya Teknolojia ambayo imekuwa kivutio kikubwa katika maonesho haya ni mfumo wa kidigitali wa kumwezesha mfugaji wa Nyuki kupata taarifa za maendeleo ya mzinga wake ikiwa ni pamoja na kujua muda muafaka asali inapokuwa tayari kwa ajili ya kuvunwa kwa njia ya simu.
Miradi mingine ni pamoja na pampu ya maji inayotumika kilimo cha umwagiliaji ambayo inatumia umeme kidogo na maji kidogo, mradi wa mtambo wa ukaushaji wa mazao kwa kutumia nishati ya jua, elimu juu ya ufugaji wa kisasa wa Samaki, utengenezaji wa bidhaa kama vile sabuni, mafuta kwa kutumia mmea wa mwani, elimu juu ukulima wa kisasa na wenye tija wa mboga mboga na mingine mingi. Pamoja na miradi hii.
Chuo Kikuu cha Dodoma kimekuwa kivutio kikubwa katika maonesho hayo kwa kuwa na kikundi cha burudani kutoka idara ya Sanaa na Taaluma za Habari ambacho kimekuwa kiburudisho kikubwa kwa wananchi waliotembelea maonesho hayo.