VIJANA WASISITIZWA KUPENDA MASOMO YA HISABATI NA SAYANSI
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti ma Ushauri Elekezi, Prof.Razack Lokina, amependekeza namna bora ya ufundishaji wa masomo ya Hisabati na Sayansi kwa elimu za sekondari ili kuleta chachu kwa vijana kuendelea kupenda masomo ya Hisabati na Sayansi hasa kwa jinsia ya kike.
Rai hiyo ameitoa wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya semina elekezi kwa wawezeshaji juu ya Moduli na Miongozo ya Masomo ya Hisabati na Sayansi katika mradi unaofadhiliwa na UNICEF Tanzania . Mradi huo umejikita kuboresha ufundishaji wa Hisabati na Sayansi kwa shule za Sekondari katika Mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe, mradi huu unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Dodoma, kupitia Ndaki ya Elimu. Mafunzo hayo yameanza tarehe 20 na yanatarajiwa kukamilika 23 Septemba, 2023, katika Ndaki ya Sayansi za Komputya na Elimu Angavu, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Aidha, Prof. Lokina ameeleza umuhimu wa Hisabati, Sayansi na Teknolojia katika karne hizi ambazo matumizi ya Sayansi na Teknolojia ni makubwa hivyo huwezi kukwepa sayansi.
“ kwa sababu karne ya 21 ni ya Sayansi na Teknolojia, hatuwezi kuendelea kuwa na jamii ambayo haiwezi kufanya mambo yake kisayansi, hivyo hatuna budi kuwaimarisha vijana wetu katika ushindani kisayansi kwa kuwafanya wapende masomo ya Hisabati ya Sayansi”
Nisitize tu kwa vijana kwamba hamna somo gumu unapoamua kulisoma, tuna vijana wanafanya vizuri masomo ya Sayansi na Hisabati ni masomo ya kawaida ila ile dhana unayokuwa nayo kichwani kwamba masomo ya Sayansi ni magumu ndo inayopelekea watu wengi kuogopa masomo ya Sayansi na Hisabati”
Naye kaimu Rasi wa Ndaki ya Elimu Dkt. Abdallah Seni, amesema matarajio ya mradi huu ni kuongeza wanafunzi wengi kupenda masomo ya Hisabati na Sayansi na hivyo wanatoa mafunzo kwa wakufunzi na walimu ili kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto zilizopo wakati wa ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Hisabati na Sayansi kwa Wanafunzi wa Elimu ya Sekondari
Pia kiongozi Mkuu wa Mradi toka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt.Rose Matete Ameipongeza UNICEF Tanzania kwa kutoa ufadhili ambao utakuwa ni mwendelezo wa kutoa mafunzo kwa walimu ili kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi kupenda masomo ya Hisabati na Sayansi.