MKUU WA CHUO KIKUU CHA DODOMA AFURAHISHWA NA MAENDELEO YA CHUO


  • 1 year
  • Office of The Chancellor

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax, ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, amesema amefurahishwa na namna Chuo Kikuu cha Dodoma kinavyoendelea kupiga hatua kutokana na tuzo mbalimbali inazojipatia katika maeneo ya Sayansi na Teknolojia, Sheria na Afya. 

 
Hayo ameyasema leo katika ukumbi wa Kimataifa wa AICC, Arusha, alipokutana kufanya mazungumzo na Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma, lililokutana kwa kikao kazi cha siku tatu na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya Utawala na Menejimenti, pamoja na kuweka mikakati ya namna litakavyosimamia majukumu yake katika kuhakikisha Chuo kinafikia malengo.
 
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya mazungumzo na Baraza hilo, Mhe. Tax, amewapongeza wajumbe wa Baraza kwa kuaminiwa kushika nyadhifa hizo na kuwataka kuisimamia vema Menejimenti ya Chuo ili kuweza kuwa mitaala inayoendana na mahitaji ya soko pamoja na kulinda maalidili ya kitanzania kwa wanafunzi wanapokuwa masomoni.
 
“Kama mnavyofahamu kuwekuwa na mmonyoko mkubwa wa maadili katika jamii, hivyo niwaombe kusimamia vema suala la utovu wa nidhamu na maadili ya chuo chetu, kwa kuipa kipaumbele Kamati ya Maadili, sambamba na kusimamia Sheria, kanuni na taratibu katika kuendesha Chuo" alisisitiza.
 
Amesema katika kipindi hiki cha mageuzi makubwa ya Nne ya Viwanda Duniani, Serikali ina mategemeo makubwa na vyuo vyetu katika kuzalisha wataalamu wenye ubora katika ushindani wa kidunia, hivyo kusisitiza ubunifu katika programu zinazoanzishwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia na uchumi wa kidigitali, kukuza vipaji na kuongeza udahili ili kuwa matokeo yanayotakiwa. 
 
Naye Mwenyekiti wa Baraza hilo Prof. Rwekaza Mukandara, akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Chuo, amesema, mafunzo ya siku tatu waliyoyapata yatasaidia kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza katika kufanya kazi kwa weledi na maarifa katika kuhakikisha malengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma yanafikiwa, ikiwemo kuwa Chuo Bora Barani Afrika kwa kulinda nidhamu na kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
 
Akitoa taarifa yake, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka, amemhakikishia Mkuu wa Chuo, Menejimenti kuendelea kushirikiana na Baraza katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kuanzisha Chuo hicho inafikiwa ikiwa ni pamoja na kuzalisha wataalamu wenye ubobevu na ushindani katika soko.
 
Kikao kazi cha siku tatu cha Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma kimefanyika huku msisitizo mkubwa ukiwekwa katika utendaji wenye matokeo na kuzalisha watalaamu bora watakaoajiriwa na kujiajiri, kwa kila upande kutimiza wajibu wake.
Comments
Send a Comment