MKAWE WAWIKILISHI WAZURI WA TAIFA


  • 1 year
  • Directorate of Students Services

Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Justin Ntalikwa amewataka wanafunzi wanaoenda kushiriki mchezo wa mpira wa kikapu Uganda kuwa wawakilishi wazuri wa Taifa ili kuleta matokeo chanya katika michezo

Prof.Ntalikwa ameyasema hayo tarehe 3 Oktoba, 2023 alipokuwa anawaaga wanafunzi ambao wanaenda kushiriki mashindano ya vyuo vikuu vya Afrika Mashariki ambayo yanafanyika Nchini Uganda katika Chuo cha Makerere kuanzia tarehe 6-9 Oktoba, 2023. UDOM inashiriki mchezo wa mpira wa kikapu wanaume.

Pamoja na mambo mengine Prof. Ntalikwa amewapongeza wanafunzi wote ambao wamepata nafasi ya kushiriki mashindano hayo na kuwaasa kuwa na nidhamu na kurudi na ushindi kwani wamebeba jukumu la kuwakilisha chuo na Tanzania kwa kuwa UDOM ndo chuo pekee kinachoenda kushiriki kutoka nchini Tanzania

"Tuwaombe mkawe washiriki wazuri wenye kushindana hatuwezi kwenda kusindikiza tuwe na ari ya kupata ushindi ili chuo chetu kiweze kusifika na kutambulika kitaifa na Kimatifa"

Naye mkufunzi wa michezo Chuo Kikuu cha Dodoma Bwn.Deogratius Mdemu ameshukuru Menejimenti ya chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuwapa nafasi wanafunzi kushiriki michezo hiyo kwa kuwa inawapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao lakini pia kujifunza toka kwa wanafunzi wengine ili kuendelea kuinua michezo chuoni na kwa Taifa.

Safari hiyo inahusisha wanafunzi 10 pamoja na wafanyakazi 3 toka chuo kikuu cha Dodoma .
 

Comments
Send a Comment