VIONGOZI WASISITIZWA KUENDELEA KUWA WAADILIFU


  • 11 months
  • Office of The Chancellor

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka amesitiza watumishi wa Chuo kikuu cha Dodoma kuendelea kuwa waadilifu kwenye majukumu yao ya kila siku na kuwa hatavumilia kwa watumishi ambao wanaenda kinyume na miongozo ya sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Prof. Kusiluka ametoa rai hiyo tarehe 13 Novemba, 2023 wakati akizindua kamati ya kudhibiti Uadilifu na kupambana na Rushwa ambayo ilihusisha viongozi wakuu kutoka vitengo mbalimbali chuoni hapo pamoja na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Prof. Kusiluka alisema “tukiwa kama taasisi ya elimu ya juu tunao wajibu wa kawaida kama taasisi nyingine wa kuzingatia maadili na kufanya kazi kwa uadilifu lakini pia tunalo jukumu jingine kubwa na ambalo umma unatupima mara kwa mara kuhusu ufanisi wetu ambao ni kuhakikisha kwamba tunawatayarisha vijana wetu kwanza kuwa na ujuzi, kuwa na maarifa lakini pia kuwa wazalendo kwa ajili ya nchi hii”

Aidha, mwakilishi wa kamishna ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bwn. Salvatory Kilasara, akitoa neno la utangulizi amewakumbusha watumishi wa chuo kikuu cha Dodoma kuendeleza maadili mazuri na kuwa mfano mzuri kwa jamii,na kuwahimiza viongozi kuheshimu kamati ya maadili kwani ni chombo muhimu sana kinachosadia kuwepo uadilifu mahala pa kazi.

Naye, Bi. Idda M. Siriwa Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma.Amesema ikiwa Chuo kikuu cha Dodoma ni chuo mojawapo ambacho kinaandaa watumishi wa umma wa badaye ni vizuri kuwapa mafunzo ya kuzuia na kupambana na rushwa ili kujenga viongozi ambao watakuwa waadilifu na hatimaye kujenga kizazi chenye maadili kitakachotenda haki na kuleta maendeleo ya nchi.

Baada ya uzinduzi,mafunzo hayo yataendelea ndani ya siku 7 kwa Ndaki, Shule kuu na Tassisi na matarajio yake ni kufika wafanyakazi 1300 na wanafuzi zaidi ya 10,000.

Comments
Send a Comment