MRADI WA HEET WAZINOA KAMATI ZA KISEKTA ZA VYUO VIKUU


  • 7 months
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeshiriki kikao cha kitaifa cha Kamati za Ushauri za Kisekta (Industrial Advisory Committee) chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaoongozwa na Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia (WyEST).


Akifungua kikao hicho Mratibu wa mradi kutoka WyEST, Dkt. Kenneth Hosea ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu, alieleza lengo la mkutano huo kuwa ni kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa Kamati za Ushauri za kisekta kutoka kila Taasisi ya Elimu ya Juu, na wadau wanaozotekeleza mradi wa HEET. Uelewa huu wa pamoja unalenga kuzisaidia kamati hizo kutoa ushauri wa kina katika utekelezaji wa mradi, kwa kuboresha na kuandaa mitaala bora itakayokidhi mahitaji ya soko la ajira na hivyo kuwawezesha wahitimu kujiajiri badala ya kutafuta ajira.


Dkt. Hosea aliongezea kuwa lengo la mradi ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini kwa asilimia thelathini (30%). Aidha, alisisitiza
kwamba kupitia mradi wa HEET, kampasi mpya zitaanzishwa katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kuongeza wigo wa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Elimu ya Juu, kutatua changamoto zilizopo katika jamii pamoja na kuandaa mitaala inayokidhi mahitaji ya jamii husika.


Kwa upande wake, mratibu wa Kamati za Ushauri za Sekta kutoka WyEST, Dkt. Hadija Kweka, alisema kuwa mbali na kushauri juu ya uhuishaji na uandaaji wa mitaala, kamati hizi pia zitatoa ushauri kwa taasisi za elimu ya juu ili kutumia sekta katika kufanya utafiti na ubunifu wa kutatua changamoto za jamii. Dkt. Kweka aliongeza kuwa taasisi za elimu ya juu zinapaswa kujenga ushirikiano endelevu na taasisi na makampuni mbalimbali ili kudumisha uhusiano huo hata baada ya mradi kukamilika, ikiwemo kuwa na maeneo ya mafunzo kwa vitendo kwa wahadhiri na wanafunzi.

Katika kikao hicho, mada kadhaa zilijadiliwa, ikiwa ni pamoja na jukumu la kamati za sekta katika kuwawezesha wanafunzi na wahadhiri kupata fursa za mafunzo ya vitendo kwa muda mrefu na yenye tija, umuhimu wa kushirikisha wadau katika maandalizi na utekelezaji wa mitaala, na umuhimu wa kutumia sekta katika kufanya tafiti na uvumbuzi wa kutatua matatizo ya jamii. Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ni mradi wa miaka mitano (5) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na unaolenga kukuza uchumi kupitia elimu ya juu.

Comments
Send a Comment