UDOM YATOA ELIMU YA MATUMIZI YA MAKTABA


  • 8 months
  • Directorate of Library Services

Kurugenzi ya Huduma za Maktaba Chuo Kikuu cha Dodoma katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi, 2024 imeungana na wanawake wengine Duniani kuadhimisha siku hiyo kwa kutembelea Shule ya Sekondari Dodoma ambapo walikutana na wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita wanaosoma mchepuo wa masomo ya Sayansi na Sanaa.

Akizungumza wakati akitoa neno la utangulizi Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Grace Msoffe, alisema lengo la kufika shuleni hapo ni kuhamasisha juu ya umuhimu wa matumizi ya huduma za maktaba pamoja na kutambulisha programu mbalimbali zinazotolewa na UDOM.

"Ninaamini kabisa mnafahamu uhusiano mkubwa uliopo kati ya maktaba na masomo, maktaba na ufundishaji, maktaba na ujifunzaji. Chuo Kikuu cha Dodoma ni chuo kikubwa sana kwa maana ya kwamba tuna programu nyingi za Sanaa na Sayansi ambapo nyie wote hapa mnaosoma masomo hayo mna fursa kubwa ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dodoma" alisisitiza Dkt. Msoffe .

Naye Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Francis Tumaini, ambaye pia ni Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2014 Shahada ya Umahiri katika Taaluma za Maendeleo amefurahia mashirikiano ambayo Chuo Kikuu cha Dodoma kimekuwa kinafanya katika shule hiyo na ameshukuru kwa msaada walioupata toka UDOM na ameuomba Uongozi wa Chuo kuwaandalia ziara wanafunzi wa kidato cha sita ambao utakuwa utaratibu unaofanyika kila mwaka kwa lengo la kujifunza zaidi.

Naye Bi. Neema Michael mwanafunzi wa kidato cha Sita mchepuo wa masomo ya Sayansi ( PCM) alisema kuwa alikuwa hajafikiria kusoma UDOM lakini kutokana na hamasa na ufafanuzi mzuri wa jinsi ya kujiunga na Chuo hicho amevutiwa na ameahidi kuwa baada ya kumaliza masomo yake atajiunga na UDOM.
 

Comments
Send a Comment