VIONGOZI WA CHUO KIKUU CHA DODOMA WAHIMIZWA KUZINGATIA MIONGOZO KATIKA KUFANYA MAAMUZI


  • 1 month
  • The University of Dodoma

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, amewataka viongozi wa chuo hicho kuzingatia miongozo, kanuni, sheria na taratibu katika utendaji kazi wao wa kila siku na hasa kwenye kufanya maamuzi ili kuimarisha utendaji wa kila siku wa taasisi na kuleta tija katika shughuli wanazosimamia.

Hayo ameyasema Jumatatu tarehe 11 Machi, 2024, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya viongozi wa chuo hicho kuanzia ngazi ya Wakuu wa Idara, RASI wa Ndaki, Amidi wa Shule Kuu, Wakurugenzi wa Taasisi, Wakurugenzi wa Kurugenzi za uendeshaji na Vitengo.

Aidha, ametaka viongozi hao kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja wa ndani na nje, kuwa wabunifu katika uandishi wa miradi na kusimamia ufanyaji wa Tafiti zenye tija ili kuongeza mapato ya chuo, pamoja na kusimamia kwa karibu tafiti za wanafunzi kwa ngazi zote; Shahada za Awali na Shahada za Umahili, ili wanafunzi kuhitimu kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Naye Prof. Timothy E. Simalenga, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma Chuo Kikuu cha Mt. John – Dodoma, Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, amewataka, viongozi wa UDOM wakati wote kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utendaji unaoakisi malengo makuu ya chuo, mgawanyo wa majukumu, na malengo mapana ya Serikali, kwa kutumia nyenzo mbalimbali na miongozo iliyoandaliwa kufikia malengo.

“Zingatieni muda na mtumie vema muda mnaopewa na Serikali katika kutekeleza majukumu yenu. Kila mmoja atambue anao wajibu wa kulinda Dira na Dhima ya Chuo, na kupitia hilo kila mmoja atambue anao wajibu wa kukitangaza chuo kutokana na shughuli anazozisimamia na kuzifanya kila siku” alisisitiza Prof. Simalenga.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yanafanyika katika Hoteli ya Mt. Gasper Dodoma, ambapo viongozi hao wanapatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali ya uongozi, ikiwemo Wajibu wa Viongozi Kitaaluma katika kutoa huduma Bora, Wajibu wa Kiongozi na Maadili katika Utumishi wa Umma, Wajibu wa Viongozi kwenye Vita dhidi ya Rushwa, Usalama wa Taarifa na Utunzaji wa Kumbukumbu n.k

Comments
Send a Comment