WANATAALUMA UDOM WAJENGEWA UWEZO KATIKA KUANDIKA MIRADI, MACHAPISHO NA TAFITI


  • 4 weeks
  • Geography and Environmental Studies

Chuo Kikuu cha Dodoma kupitia Idara ya Jiografia na Stadi za Mazingira tarehe 25 Machi 2024 kimeanza mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wanataaluma na watafiti wa Chuo hicho katika uandishi wa miradi mikubwa ya Utafiti.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Warsha hiyo Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka, amewataka watafiti wa Chuo hicho kuongeza jitihada katika kutafuta fursa za Utafiti, kwa kutambua kila mwanataaluma anao wajibu wa kufanya Utafiti, Wajibu wa Menejimenti ni kuwaongezea maarifa na kuwapa ushirikiano pale unapohitajika ili kuandika maandiko yaliyo bora kwa manufaa ya Chuo na Taifa kwa ujumla.

"Lengo letu ni kuongeza wigo wa wanataaluma wetu na watafiti wetu ambao wanaweza kuandika kazi nzuri ambazo zinakubalika kimataifa na kukubalika kimataifa maana yake UDOM itatambulika na Wanataaluma na Watafiti wenyewe watatambulika " Alisisitiza Prof. Kusiluka

Naye, Mkuu wa Idara ya Jiografia na Stadi za Mazingira Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Augustino Mwakipesile, amesema kwa sasa kumeibuka wimbi ambalo maandiko ya watafiti wengi hayafikishwi sehemu sahihi hivyo kupelekea kukataliwa kwa machapisho mengi, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuwaongezea maarifa ya kujua vyanzo sahihi vya kupeleka maandiko yao ndani na nje ya nchi.

Profesa wa Tafiti kutoka Chuo Kikuu cha Barcelona, Prof. Dan Brockington ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo amesema kazi za utafiti na kuandika zinahitaji jitihada kubwa, hivyo kila mtafiti anahitaji namna nzuri ya kushirikiana na watafiti wengine ili kupata uzoefu mkubwa na kiu yake ni kuona watafiti toka Chuo Kikuu cha Dodoma wanajulikana Dunia nzima.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushirikisha wanataaluma wa Ndani na nje ya nchi.

Comments
Send a Comment