UDOM YAPIMA AFYA BURE CHAMWINO


  • 7 months
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa pamoja na Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii imezindua zoezi uchunguzi wa afya na kuongeza ufahamu wa umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya ili  kupunguza athari za magonjwa na matatizo yatokanayo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika Hospitali ya UHURU iliyopo wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.

Zoezi hilo litakalofanyika kwa siku mbili ni muendelezo wa matukio yanayofanywa na UDOM kuelekea mkutano wa kwanza wa kimataifa wa maswala ya Afya unaoitwa “UDOM Scientific Conference on Health (USCHe)” utakaofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Mei, 2024 katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma uliopo mji wa Serikali Mtumba.

Akizungumza katika ufunguzi wa zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa, anaamini zoezi hilo litasaidia wananchi kujua namna ya kutunza afya zao pamoja na athari za magonjwa yasioambukiza kama vile magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, shinikizo la juu la damu (hypertension), magonjwa ya mapafu na magonjwa ya figo, macho, pua, koo, afya ya kinywa, pamoja na kiribatumbo. 

“Vyuo Vikuu kama vituo vya uchunguzi na uvumbuzi vya masuala yanayohusiana na afya na ukuzaji wa rasilimali watu ya nchi, ni moja ya sekta muhimu katika kufikia lengo la tatu la maendeleo endelevu la Umoja wa Mataifa kuhusu maisha yenye afya na ustawi kwa wote.” Aliongeza Mhe. Senyamule.

Mhe. Senyamule aliomba uongozi wa UDOM kuongeza siku moja katika zoezi hili ili waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Naye Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Albino Tenge amesema kuwa, Chuo Kikuu Cha Dodoma kama mdau wa Afya, kitaendelea kutoa elimu kwa watanzania kuhusu kujikinga na magonjwa pamoja na elimu juu ya matibabu sahihi na ya uhakika hapa nchini husani mkoani Dodoma.

“Watalaamu wetu wa afya kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma wakiwemo madaktari bingwa, wataalam wa afya ya Jamii na lishe tutaendelea kufanya kampeni hizi za uchunguzi na kampeni zingine za matibabu kuhakikisha jamii inaelimishwa ipasavyo ili kuzuia  magonjwa pamoja na kugundua dalili za mapema.” Alisisitiza Prof. Tenge

Mnufaika wa huduma hii ndugu Rehema Mahendoni amekishukuru Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kupeleka wataalamu wa huduma ya upimaji afya kwani imewasaidia wananchi wengi wa wilaya ya Chamwino wenye kipato cha chini kupima vipimo hivyo bila gharama yoyote.

“Mimi ninashukuru sana kwa kutuletea huduma hii ambayo imetusadia kujua afya zetu hasa sisi wenye kipato kidogo”.

Zoezi hili ni muendelezo wa utekelezaji wa majukumu makuu ya Chuo ya kutoa huduma kwa jamii ambapo kuanzia tarehe 13 machi hadi tarehe 15 Machi, 2024 katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Figo Duniani UDOM ilipima afya wananchi 793, na kwa siku hizi mbili wilayani Chamwino inategemewa wananchi 1,000 kufikiwa na huduma hii.

Comments
Send a Comment