CHUO KIKUU CHA DODOMA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA CHUO KIKUU CHA UUGUZI RUTGERS CHA NCHINI MAREKANI


  • 10 months
  • The University of Dodoma

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, leo amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha uuguzi Rutgers cha nchini Marekani, ambao ni wadau muhimu wa maendeleo wa chuo hicho kupitia Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii.

Akikaribisha ujumbe huo, Prof. Kusiluka ameelezea shukrani zake kwa ushirikiano na ufadhili unaotolewa na Chuo Kikuu cha Rutgers kwa Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Dodoma, amesisisitiza matarajio makubwa ya UDOM katika kuendeleza kuanzisha miradi mingi zaidi ya kujifunza na ufundishaji, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kozi mpya za uuguzi na Afya ya Jamii.

"Kwa kuzingatia ongezeko la matumizi ya teknolojia nchini na uwekezaji mkubwa tulioufanya katika miundombinu ya TEHAMA, sioni sababu ya kutokufundisha baadhi ya programu kwa njia ya masafa kwa kushirikiana na wataalamu wenzetu waliopo Rutgers" alisema Prof. Kusiluka.

Aidha, aliwataka viongozi wa Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii, kutumia fursa zilizopo katika kuanzisha kozi ambazo zitakuwa na manufaa kwa taifa na zinazoweza kufundishwa kupitia mtandao.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Rutgers, Dkt. Emilia Iwk, alieleza kuwa kupitia ushirikiano uliopo kati ya vyuo hivyo viwili, wamepanga kuongeza maeneo ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dodoma ili kuongeza ujuzi na kupanua wigo wa mafunzo kwa wanachuo.

Kwa sasa, Chuo Kikuu cha Dodoma kina ushirikiano na Chuo Kikuu cha Rutgers katika maeneo ya uandishi wa miradi ya pamoja ya utafiti, ufundishaji, ubunifu, na kubuni mitaala mipya ya masomo.

Ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Rutgers uliongozwa na Dkt. Emilia Iwk, akifuatana na viongozi wengine Dkt. Antony Fillipelli na Bi. Catie Filippeli Apn, pamoja na wanafunzi 12 wanaosoma katika chuo hicho ambao wamekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu na wanafunzi wenzao katika Shule Kuu ya Uuguzi na Tiba ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mkuu wa Idara ya “Clinical Nursing” ya Chuo Kikuu cha Dodoma Bi. Angelina Alphonce Joho, ameeleza ujumbe huo utakuwepo nchini kwa majuma kadhaa, ambapo mbali na kufundisha, pia wamepanga kufanya tathmini ya maeneo ya ushirikiano pamoja na kuainisha maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo kuangalia uwezekano wa kupata vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kufundishia pamoja na fursa za mafunzo wa wakufunzi ili kuendelea kuwajengea uwezo.

Comments
Send a Comment