SERIKALI YA WANAFUNZI (UDOSO) YANOLEWA KIMADILI
Viongozi wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma wameaswa kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia maadili, nidhamu na uwajibikaji.
Ushauri huo umetolewa tarehe 8 Januari, 2024 na makamu mkuu wa chuo kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka wakati akizungumza na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO) na wanafunzi wa shahada za juu za uzamili na uzamivu kwenye ukumbi wa mikutano, ndaki ya sayansi za kompyuta na elimu angavu (CIVE).
Prof. Kusiluka pia amewatoa wasiwasi viongozi na wanafunzi hao kutokatishwa tamaa na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kipindi cha uongozi wao na kujadiliana nao kwa pamoja juu ya mikakati ya maendeleo na matarajio ya chuo kwa mwaka mpya wa 2024.
Aidha, Prof. Kusiluka amewapongeza viongozi hao wa UDOSO kwa kuendelea kusaidia uongozi wa chuo katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo,usawa wa kijinsia, Michezo pia na kwa kujitoa kwa moyo kuwawakilisha wanafunzi wenzao.
Aidha, rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma(UDOSO) Ndg, Godfrey Gilagu ameishukuru menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuendelea kusikiliza changamoto zinazokabili wanafunzi na kuzitatua, na kwa upande wao wameahidi kuendelea kukumbusha wanafunzi wenzao namna sahihi ya kuwasilisha maoni na changamoto pindi zinapojitokeza.