UDOM YAADHIMISHA MIAKA 60 YA MUUNGANO KWA KUPANDA MITI
Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma imeaswa kutunza miti iliyopandwa ili kuendana na lengo la kukijanisha Dodoma. Rai hiyo imetolewa leo tarehe 27 Januari 2024, na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Hamis Mkanachi, alipomuwakilisha Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, kwenye zoezi la upandaji miti ikiwa ni kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Dkt. Mkanachi amesema kuwa zoezi la upandaji miti ni lazima liendane na mikakati ya kutunza miti ili kuwe na maana ya zoezi hilo na tafsiri halisi ya kukijanisha Dodoma.
Dkt. Mkanachi pia ameelekeza Wakala wa Huduma za Misitu kuongeza uzalishaji wa miche ili kuendana na lengo la upandaji wa miti milioni 40 kwa mkoa wa Dodoma.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, ameishukuru Serikali kwa kuteua Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa sehemu ya kupanda miti kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano na kwamba UDOM itaendelea kuwa kinara katika Kampeni ya Kukijanisha Dodoma.
Prof. Kusiluka aliongeza kuwa UDOM inafurahi kusheherekea siku ya kuzaliwa ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupanda miti huku akiongoza wadau wa mazingira kumuimbia Mhe. Rais wimbo wa kumtakia Heri ya Siku ya Kuzaliwa.
Zoezi hilo limefanyika kwenye eneo la ukanda wa kijani la Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo jumla ya miti 1,000 imepandwa. Chuo Kikuu cha Dodoma kimepanga kupanda miti elfu 30,000 mwaka huu ambapo jumla ya miti 11,500 imeshapandwa.