UDOM KUIMARISHA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI WA HISABATI NA MASOMO YA SAYANSI-KIGOMA


  • 8 months
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza kutoa mafunzo ya siku nne kwa Walimu wanaofundisha Hisabati na Masomo ya Sayansi katika Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma kupitia mradi unaofadhiliwa na UNICEF ambao umejikita kuimarisha viwango vya Ujifunzaji na Ufundishaji wa Hisabati na masomo ya Sayansi shule za Sekondari katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe.

Mafunzo hayo ambayo yameanza tarehe 19 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 22 Februari, 2024, yanafanyika Chuo cha Ualimu Kasulu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri kwa Umma Prof. Razack Lokina amewapongeza walimu kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya kuhakikisha ufaulu wa masomo ya Sayansi na Hisabati unakuwa mkubwa na ametoa hamasa kwa Walimu kuendelea kutoa msisitizo kwa wanafunzi wengi wa kike kupenda na kusoma masomo ya Sayansi kwani katika karne hii maendeleo yoyote yanagemea matumizi ya Sayansi na Teknolojia.

Naye kiongozi Mkuu wa Mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt.Rose Matete, amesema kutokana na uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati mafunzo hayo yatasaidia kuongeza na kuinua viwango vya ujifunzaji na ufundishaji wa Hisabati na Masomo ya Sayansi sambamda na kuhakikisha Walimu wanatumia teknolojia wanapofundisha masomo hayo ili kufanya wanafunzi kupenda kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati.

Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mwl. Iyogo Isujwe, kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma, ameipongeza UDOM kwa kutoa mafunzo hayo kwani yatasaidia na kuimarisha uwezo wa walimu na kusaidia wanafunzi wengi kuvutiwa kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati.

Mafunzo hayo yataendelea katika mkoa wa Songwe na Tabora ili kuendelea kuhimiza ushiriki mzuri wa wasichana katika masomo ya Hisabati na Sayansi, kukuza Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) kama zana ya ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Hisabati na Sayansi katika Shule za Sekondari pamoja na kuimarisha muunganisho wa masuala ya mabadiliko ya Tabia nchi katika ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Hisabati na Sayansi kwa Shule za Sekondari.
 

Comments
Send a Comment