LUGHA ITUMIKE KUIMARISHA UHUSIANO KATI YA TANZANIA NA CHINA


  • 3 weeks
  • The University of Dodoma
Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian ametoa wito juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili na Kichina katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na China.
 
Mhe. Balozi ameyasema hayo tarehe 24.10.2024 katika hafla ya utoaji wa tuzo za balozi wa China iliyofanyika katika ubalozi wa China Dar es Salaam Tanzania ambapo jumla ya wanafunzi na wahadhiri 11 kutoka UDOM wamepata tuzo hiyo ya umahiri katika Lugha ya Kichina.
 
Mhe. Chen aliongeza kuwa, Tanzania na China anaadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa Kidiplomasia huku kukiwa na mafanikio makubwa katika Sekta za Uchumi, Utamaduni na Elimu huku akitaja baadhi ya mafanikio katika sekta ya elimu kuwa ni uingizwaji wa lugha ya Kichina katika mitaala na sera ya elimu nchini Tanzania hivyo Kichina kufundishwa kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi Vyuo Vikuu.
 
Aidha aliongeza kuwa, lugha za Kiswahili kufundishwa katika baadhi ya Vyuo Vikuu nchini China ni sehemu ya mafanikio hayo.
 
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa, tunapoadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya China na Tanzania, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi ya Teknolojia inatambua umuhimu wa ushirikiano huu katika kukuza sekta ya Elimu nchini. Alitaja baadhi ya mafanikio ya uhusiano huu ni pamoja na mabadilishano ya waalimu, upatikanaji wa ajira kwa wahitimu, ufadhili wa masomo nchini China na misaada ya miundombinu ya kujifunzia.
 
Prof. Nombo aliongeza kuwa, kutokana na mabadiliko na mitaala na sera ya elimu nchini Tanzania, lugha ya Kichina inafundishwa kuanzia ngazi ya msingi hadi Chuo Kikuu na imekuwa chanzo cha ajira kwa wahitimu wengi hivyo kutoa wito kwa vijana kujifunza lugha ya Kichina.
 
Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika hafla hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shahada za Awali Dkt. Victor George amesema kuwa, tuzo hii imekuwa chachu kwa Wanafunzi kujifunza lugha ya Kichina kwa bidii zaidi na hivyo kufanya vizuri katika masomo yao. Ametoa wito kwa wanafunzi wanaojiunga na Vyuo Vikuu kusoma Lugha na Utamaduni wa Kichina ili waweze kufaidi fursa mbalimbali zinazotolewa kwa wanafunzi wanaosoma lugha hiyo.
 
Bw. John Gerald Waritu ambaye ni mmoja wa wanufaika wa tuzo hiyo kutoka UDOM ameushukuru Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na waalimu wake kwani wamekuwa chanzo cha yeye kupata tuzo hiyo.
 
Naye Bi. Monica Masongoni Fumbo ambaye amemaliza masomo yake ya Shahada ya Awali katika lugha ya Kichina UDOM, ambaye pia ni mnufaika wa tuzo hii almesema kuwa alipata ajira hata kabla ya kumaliza masomo yake.
 
Tuzo ya balozi wa China nchini Tanzania imeanza kutolewa mwaka 2018 na kwa mwaka 2024 jumla ya wanafunzi na waalimu 132 wamepata tuzo hiyo.
Comments
Send a Comment