PROF. KUSILUKA AWAASA WANAFUNZI UDOM
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Prof. Lughano Kusiluka amewapongeza na kuwaasa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na UDOM mwaka wa masomo 2024/25 kuzingatia lengo kuu lililowaleta chuoni ambalo ni kusoma kwa bidii, ili waweze kuhitimu vizuri na kwa wakati kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla .
Prof. Kusiluka aliyasema hayo katika Semina Elekezi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 2024/25 inayofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga UDOM kuanzia tarehe 31 Oktoba, 2024 hadi tarehe 1 Novemba, 2024.
Aliwakumbusha kuzingatia mila na desturi za kitanzania kama vile kuvaa nguo za heshima, kujiepusha na matumizi na dawa za kulevya, ushoga, kamari, unywaji wa pombe pamoja na mimba zisizotarajiwa.
"Kesho yako inategemea kwa kiasi kikubwa mtindo wako wa sasa wa maisha na kujituma ukiwa chuoni. Wanafunzi wengi wanafeli kutokana na kushindwa kutumia muda wao vizuri na sio kwasababu ya kuwa na uwezo mdogo wa kiakili," aliongeza Prof. Kusilika.
Naye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo -Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina amewataka wanafunzi kuzingatia muda, kusoma kwa bidii na kuhudhuria darasani. Pia amewahimiza kufuata taratibu zilizowekwa pale wanapohitaji kuahirisha mitihani au kusitisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha na Utawala Prof. Winester Anderson, amewaasa wanafunzi kufuata Sheria, Kanuni na Utaratibu uliowekwa na chuo, katika kipindi chote cha masomo.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi (UDOSO) Bw. Mohamed Abdallah Mohamed amewataka wanafunzi kujua malengo yao, pamoja na mipaka yao. Pia, amewasisitiza kuwasiliana na uongozi wa serikali ya wanafunzi ambao unaanzia katika ngazi ya kiongozi wa darasa, bweni, bunge, gavana, waziri hadi kufikia ngazi ya shirikisho.
Semina hiyo elekezi inayofanyika katika ngazi ya Chuo inahudhuriwa na wanafunzi zaidi ya elfu tano wa mwaka wa kwanza inawahusisha watoa mada kutoka ndani na nje ya Chuo. Semina hii pia itafanyika katika ngazi ya Ndaki, Shule Kuu na Taasisi za Chuo Kikuu cha Dodoma.