UDOM KIDEDEA TUZO YA TAASISI BORA NA MAHIRI KUTATUA KERO ZA WANANCHI
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimetangwazwa mshindi wa tuzo ya Taasisi bora za Serikali yenye muitikio wa haraka na mwajibikaji kwa jamii hasa katika kutatua Changamoto na kero zinazoibuliwa na wananchi kwa njia ya Mtandao.
Tuzo hiyo iliyolewa Jumamosi tarehe 21 Septemba na Asasi ya Kiraia ya Jamii Forums, wakati wa sherehe mahusisi ya utoaji Tuzo hizo kwa mwaka 2024, iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana na kuhudhuriwa na wageni mbali mbali wa Ndani na nje, wakiwemo wawakilishi wa Wananchi.
UDOM imeshinda tuzo hiyo katika kuhitimisha mashindano ya habari bora yenye kuchochea mabadiliko 'stories of Changes’ yanayofanyika kila mwaka kwa kuratibiwa na Jamii Forum na washirika wake, kwa lengo la kutoa fursa kwa wananchi kuibua hoja zenye kuchochea mabadiliko na kutatua changamoto zilizopo katika Jamii.
Akifafanua namna Jamii forum ilivyopata washindi wa Tuzo hizo; Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Bw. Maxence Melo, amesema Taasisi 10 za Serikali zilizopata Tuzo hiyo UDOM miongoni, zimechaguliwa na wananchi kwa kuwa mstari wa mbele kujibu hoja za wananchi kila zinapoibuliwa kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na kutoa mrejesho kwa wakati kuhusu hatua ilizozichukua katika kutatua kero hizo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Kitengo Cha Mawasiliano na Masoko-UDOM, Bi. Rose Joseph, ameishukuru Asasi ya Jamii Forum kwa kutambua mchango wa UDOM katika kuhabarisha Umma, na kwamba Tuzo hiyo ni alama kwamba wananchi wanathamini na kutambua kazi kubwa inayofanywa na UDOM, na kuahidi kuendelea kutoa taarifa na kujibu kero za wananchi kwa wakati ili wananchi waendelee kunufaika na huduma zinazotolewa na Chuo hicho.
"Kwetu sisi hili ni deni kubwa kwa wananchi. Niendelee kutoa wito kwa wananchi kuendelea kujenga Imani na Chuo chetu kwani tumejizatiti kuhakikisha Wanafunzi wanaopata bahati ya kusoma chuoni kwetu wanapata huduma bora na za uhakika wakati wote. Kwa kutumia teknolojia tutahakikisha tunakufikia na kuwahudumia ipasavyo, alisisitiza Bi. Rose
Aidha,ameishukuru Jamii Forum kwa kutambua juhudi za UDOM na kuahidi ushirikiano zaidi kwa maslahi makubwa ya Taifa katika kuendeleza sekta ya Elimu ya Juu nchini.