UTETEZI WA PhD UDOM WAANZA KUFANYIKA KWA NJIA YA MTANDAO


  • 6 days
  • The University of Dodoma

Kwa mara ya kwanza tarehe 27 Septemba, 2024 Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza kufanya utetezi wa PhD kwa njia ya mtandao na Bw. Netho Ndilitho kutoka Ndaki ya Biashara na Uchumi Idara ya Uchumi amekuwa mwanafunzi wa kwanza kutetea tafiti yake kwa njia ya mtandao (Zoom Meeting).

Akizunguanza wakati wa wasilisho hilo, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Biashara na Uchumi Prof. Ismail J. Ismail amesema utetezi wa tasnifu utakaokuwa ukifanyika kwa njia ya mtandao utawasaidia wananchi kupata uelewa zaidi, kwani taarifa hukusanywa kutoka kwao na baada ya tafiti kukamilika watapata mrejesho. Hii itasaidia kuongeza uwazi juu ya nini hasa chuo kinafanya kama njia ya kurudisha kwa jamii, kwani wananchi wataona jinsi mwanafunzi anavyoulizwa maswali, anavyoelezea tatizo aliloliona kwenye jamii na suluhisho la kutatua changamoto hizo.

Kwa upande wake mwanafunzi wa PhD Bw. Netho Ndilitho, amesema amefurahi kuwa mwanafunzi wa kwanza kufanya utetezi wa andiko lake mubashara kupitia mtandao wa Zoom na kupongeza uongozi wa chuo kwa kutekeleza maagizo ya Serikali kwa vitendo na kwamba UDOM ni chuo kinachofanya vizuri hivyo kutoa rai kwa viongozi, watumishi wa Serikali na Sekta binafsi kujiendeleza kielimu kwa Shahada ya Uzamivu (Phd) UDOM.

Shuhuda wa tukio hilo Bi. Dorcas Gwamwanza , mwanafunzi wa Shahada ya Uzamiri kutoka UDOM amesema, uwasilishaji wa tafiti kwa njia ya mtandao utamsaidia kujiandaa vizuri na kuielewa zaidi tafiti atakayokuja kuifanya kabla ya kuiwasilisha. Pia uwasilishaji huu kwa njia ya mtandao, utasaidia watu wengi kupata taarifa kwa wakati mmoja na utunzaji wa kumbukumbu.

Chuo Kikuu cha Dodoma kimekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha kwamba matokeo yanayopatikana kwenye tafiti yanawafikia wananchi kwa njia ya kidijitali.
 

Comments
Send a Comment