CRDB YAJA NA MWAROBAINI WA USAJILI VYUONI


  • 1 day
  • The University of Dodoma
Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wamewawezesha wanafunzi wa Vyuo vya kati na juu kupata mkopo wa kujisajili usio na riba.
 
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa UNI LOAN kutoka CRDB iliyofanyika tarehe 15 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Seneti Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Prof. Peter Msofe amesema mkopo huo utawasaidia wanafunzi wengi kuweza kufanya usajili kwa wakati na amewaomba CRDB wazidi kuwasaidia wanafunzi katika kutatua changamoto mbalimbali za kifedha zinazowakabili wanafunzi wakati wa kujisajili.
 
Naye, Meneja wa Kanda ya kati CRDB Bi. Chabu Mishwaro amesema mkopo huu wa kujisajili hautakuwa na riba yoyote na mwanafunzi akiomba mkopo huu unaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya chuo husika.
 
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu Bw. Julius Bura amesema wanafunzi wengi walikuwa wakiilalamikia Bodi ya Mikopo lakini kupitia mkopo huu unaotolewa na CRDB malalamiko hayo yataisha kwasababu wanafunzi watakuwa na uhakika wa kujisajili.
 
Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Razack Lokina ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi amesema wanafunzi wengi watanufaika na mkopo huu na utasaidia kupunguza malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wanafunzi.
 
Aidha, Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Bw. Mwinyi Hussein ameipongeza CRDB na kusema mkopo huu unaenda kutatua malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wanafunzi vyuoni.
 
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa Awali na Kati kutoka CRDB amesema baadhi ya vigezo watakavyotumia kumpatia mkopo mwanafunzi ni pamoja na kuwa na akaunti ya CRDB na atatakiwa kukopa kijigitali kisha atatoa nambari ya malipo(control number) na mkopo utaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya chuo husika. Aidha, ameongeza kuwa, mkopo huo hautazidi kiasi cha Tsh. 360,000.
 
Benki ya CRDB imekuwa ikiwasaidia wanafunzi wa vyuo vikuu kupata huduma mbalimbali za kifedha na kupitia bidhaa yao mpya ya UNI LOAN wanaenda kufanya mapinduzi makubwa katika kuongeza idadi ya Wanafunzi watakaojisajili kwa wakati Vyuo Vikuu nchini.
Comments
Send a Comment