WATAALAMU UDOM KUSHIRIKIANA NA CHUO KIKUU CHA IDAHO MAREKANI KUFANYA TAFITI ZA KISAYANSI


  • 17 hours
  • The University of Dodoma
Wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Idaho nchini Marekani wamekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) tarehe 21 Oktoba, 2024 yenye lengo la kuanzisha ushirikiano katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi.
 
Akizungumza katika kikao hicho, Mwakilishi wa Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha na Utawala Prof. Wineaster Anderson amesema UDOM na Idaho vinaweza kushirikiana katika kufanya tafiti za kisayansi pamoja na mabadilishano ya wanafunzi na wahadhiri lengo likiwa kujifunza na kuongeza uelewa zaidi katika masomo ya Sayansi. 
 
Ametaja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa kufanya miradi ya pamoja na utoaji wa huduma za upandikizaji wa figo, uroto (born marrow) na matibabu ya saratani; miradi ambayo iko katika hatua mbalimbali za mazungumzo ya uanzishwaji wake na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania.
 
Kwa upande wake Prof. Luke Harmon kutoka Chuo Kikuu cha Idaho amesema kuwa, kushirikiana na kuwezesha ufundishaji kwa vitendo na matumizi ya vifaa mbalimbali vya kisayansi pamoja na kufanya semina kutasaidia kukuza uelewa kwa wanafunzi.
Naye, Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi (UDOM) Prof. Ainory Gesase amesema kuna maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na kufanya tafiti za magonjwa mbalimbali yanayoiathiri jamii yetu kama vile ugonjwa wa kisukari pamoja na tafiti zitakazowezesha upatikanaji wa maji safi. Ameongeza kuwa wahadhiri wakipatiwa maarifa ya kutosha, wataweza kuwafundisha wanafunzi kwa weledi.
 
Kaimu Amidi wa Shule Kuu ya Afya na Tiba ya Meno -UDOM, Dkt. Jumanne Shakiru, ameeleza kuwa mazungumzo haya yamekuja wakati muafaka ambapo Shule Kuu ya Sheria inaendelea kuboresha mitaala yake na kuanzisha programu mpya ya ‘Biomedical Engineering’ ambapo ushirikiano huu utasaidia katika kufanikisha uanzishwaji wa programu hii na uboreshaji wa mitaala.
 
Prof. Onesmo Balimba kutoka Chuo Kikuu cha Idaho Marekani amesema ipo haja ya kushirikiana kufanya tafiti kwenye magonjwa adimu pamoja na kuandaa mafunzo endelevu yahusuyo maswala ya kisayansi. Alieleza kuwa wanafunzi na wahadhiri wanaweza kutumia takwimu zinazopatikana mtandaoni kufanya tafiti.
 
Mazungumzo ya kuanzisha ushirikiano kati ya UDOM na Chuo Kikuu cha Idaho nchini Marekani yana lengo la kuwaongezea maarifa wanafunzi pamoja na wahadhiri wanaofundisha sayansi katika vyuo hivi.
Comments
Send a Comment