UDOM MWENYEJI KAMPENI YA MTI WANGU BIRTHDAY YANGU


  • 3 days
  • The University of Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule tarehe 18 Oktoba, 2024 amezindua kampeni iliyopewa jina la "Mti Wangu Birthday Yangu" iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), lengo likiwa kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti wakati wa kusherehekea siku zao za kuzaliwa (birthday).
 
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mhe. Senyamule amesema Dodoma kuna uharibifu mkubwa wa mazingira na njia ya kukabiliana na changamoto hiyo ni pamoja na utoaji wa elimu ya utunzaji mazingira, kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama vile gesi na umeme pamoja na kupanda miti. Aidha, amewahamasisha wananchi kupanda miti mingi wakati wa kusherehekea 'birthday' zao kama ishara ya kuunga mkono juhudi za serikali za kutunza mazingira.
 
Kwa upande wake Mwakilishi wa Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha na Utawala Prof. Wineaster Anderson amesema eneo ambalo miti imepandwa UDOM  (Jakaya Kikwete Square) lina historia ya kuwa ni eneo la katikati ya UDOM na lilitengwa  rasmi kuwa sehemu ya mapumziko.  Hivyo kupanda miti katika eneo hilo ni wakati muafaka katika kuboresha matumizi ya eneo hilo.
 
Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kasper Mmuya amesema kampeni hii ina lengo la kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na amewahimiza wananchi kupanda miti mahali popote hata kama wanaishi kwenye nyumba za kupanga. Pia, amewapongeza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa utayari wao wa  kuwapatia miti pale walipohitaji.
 
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri amesema kuna uhusiano mkubwa kati ya binadamu na mazingira kwani miti hutupatia matunda na kivuli, hivyo tuungane na serikali katika kuhakikisha tunapanda miti.
 
Takribani miti 780 imepandwa kupitia kampeni hii yenye lengo la kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha kwamba wananchi wanathamini na kutunza mazingira, ili kuweza kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.
Comments
Send a Comment