HOSPITALI YA BENJAMIN KWA USHIRIKIANO NA CHUO KIKUU CHA DODOMA KUANZA UJENZI WA KITUO CHA UMAHIRI CHA MAFUNZO NA UPANDIKISAJI FIGO


  • 3 weeks
  • The University of Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka kwa pamoja wametembelea Makao Makuu ya Shirika la Tokushukai, jijini Tokyo na kukutana na Mwenyekiti wa Shirika hilo, Prof. Shinichi Higashiue.

Katika mkutano huo, viongozi hao wamekubaliana kuanza mchakato wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo na Upandikizaji wa Figo kitakachojengwa jijini Dodoma. Kituo hicho kitaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Aidha, kuanza kwa matumizi ya teknolojia ya “robotics” katika upandikizaji figo na upasuaji wa ubongo nchini Tanzania ni suala lililojadiliwa katika kikao hicho.

Shirika la Tokushukai limeahidi kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo ambao unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka 2025. Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Baraka Luvanda pia alishiriki katika kikao hicho.

Aidha, Watendaji wa Taasisi hizo mbili wamekutana na Prof. Shuzo Kobayashi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Shonan Kamakura, ambayo ina kituo kikubwa cha usafishaji damu pamoja na teknolojia za kisasa za tiba ya saratani kwa kutumia “Proton Beam Therapy” na “Boron Neutron Capture Therapy”. Prof. Kobayashi pamoja na Prof. Tanabe Kazunari ni waanzilishi wa huduma ya upandikizaji figo jijini Dodoma ambayo ilihusishwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa mwaka 2018 baada ya kupata mafunzo nchini Japan.

Aidha , jana 23/10/2024 Prof Kusiluka na Prof Makubi walihudhuria sherehe za mazishi ya Dr.Torao Tokuda ambaye ni mwanzilishi mkuu wa Tokushukai.

Ziara hiyo pia itawakutanisha Watendaji hao na Viongozi wa za AFRECO ambacho ni Chama cha Maendeleo ya Uchumi wa Afrika nchini Japani pamoja na Taasisi ya Japani ya Ukuzaji wa Tasnia ya Uhandisi wa Vifaa Tiba ikiwa ni juhudi za kupata wataalamu na vifaa kwa ajjli ya kuanzisha mafunzo ya Shahada ya Uhandisi wa Vifaa Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
 

Comments
Send a Comment