MRADI WA HEET WATOA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MIRADI YA UJENZI UDOM


  • 5 days
  • The University of Dodoma

Timu ya wataalamu wa Ujenzi, Usalama wa Mazingira na Jamii, Ununuzi na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia (WyEST) imetoa mafunzo kwa timu ya utekelezaji wa mradi kutoka UDOM juu ya usimamizi wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa na mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

 
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 11- 15 Novemba, 2024 katika Hoteli ya Zabibu Dodoma, yamehusisha jumla ya washiriki 20 wanaosimamia eneo la Ununuzi, Usalama wa Mazingira na Jamii, Ujenzi, Mawasiliano, Fedha na Mipango pamoja na Ufuatiliaji na Tathmini.
 
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuijengea uwezo timu ya utekelezaji wa mradi kutoka UDOM katika usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi kuanzia hatua ya awali ya uandaaji wa nyaraka za manunuzi, mambo ya kuzingatia katika uandaaji na usimamizi wa mikataba, usalama wa mazingira na jamii pamoja na ufuatiliaji na tathmini ya mradi wakati wote wa utekelezaji wa mradi.
 
Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku tano, Mratibu Msaidizi wa Mradi Dkt. Happiness Nnko amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kwani UDOM imeanza utekelezaji wa miradi ya mikubwa ya ujenzi ambayo inahitaji umakini katika usimamizi. Amesema, mafunzo haya yamewezesha kuelewa sehemu ambazo zina mianya katika utekelezaji wa mradi na yamesaidia kuelewa namna ya kudhibiti mianya hiyo.
 
“Mada zilizotolewa zimetujengea uelewa na kutukumbusha mambo ya msingi hasa katika hatua za upatikanaji wa wakandarasi na imetukumbusha kwanza, tunaposaini mkataba wa mradi ni wajibu wa wasimamizi wa mradi kusimamia hadi mradi unapokamilika” Alieleza Dkt. Nnko.
 
Naye kiongozi wa majenzi katika mradi wa HEET kitaifa kutoka WyEST Mhandisi Hanington Kagiraki amesema kuwa, mafunzo hayo yalilenga kupitisha Uongozi na Wataalamu wanaosimamia mradi katika maeneo muhimu ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi pamoja na kuona uhalisia wa kile kinachofundishwa katika maeneo ya miradi ya ujenzi inayoendelea UDOM.
 
Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo Dkt. Salum Matotola amesema kuwa mafunzo yamemuwezesha kufahamu wajibu na haki za kila upande katika utekelezaji wa mradi.
 
“Mafunzo haya yameniwezesha kufahamu majukumu ya kila mmoja katika utekelezaji wa mradi na uelewa juu ya viatarishi vinavyoweza kutokea katika utekelezaji wa mradi na jinsi ya kuviepuka.” Alisema Dkt. Matotola.
 
Bw. Victor Mgendi ambaye pia ni mnufaika wa mafunzo haya ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo ameweza kuelewa namna ya kufanya mawasiliano na mshauri elekezi/mkandarasi kulingana na mkataba na namna bora ya usimamizi wa mradi utakaopelekea mradi kumalizika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
 
Washiriki na wawezeshaji wa mafunzo hayo walipata fursa ya kutembelea miradi ya ujenzi wa maabara katika Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati na madarasa katika Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi UDOM, inayotekelezwa kupitia mradi wa HEET.
 
 
 
 
ACg8ocIzQom3CVne6y0jc4yfXB-k-YnvzwNxqVe7TyMdQNNWCPo3kYUo=s40-p

ReplyForward

 
Add reaction
Comments
Send a Comment