UDOM WAPATA MAFUNZO KUHUSU HATAZA NA HATIMILIKI


  • 6 days
  • The University of Dodoma

Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Novemba 25, 2024 wameanza kupatiwa semina ya hataza (patent) pamoja na alama za biashara na huduma, kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Akifungua rasmi semina hii inayofanyikia UDOM, Mkurugenzi wa Tafiti, Machapisho na Ushauri Elekezi - Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Pendo Kasoga amesema semina hii itawasaidia wanataaluma kujua haki zao katika machapisho wanayoyaandika na miliki bunifu (Intellectual Property) wanazozivumbua. Pia, amewaomba BRELA kutoa vyeti kwa wanaohudhuria, kama motisha ya kurasimisha miliki binifu zao.

Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka BRELA, Wakili Vincensia Fugo amesema, ipo haja ya elimu kuhusu hataza (patent) pamoja na hakimiliki (copyright) kutolewa kwa jamii, ili watu waweze kulinda bunifu zao. Ameongeza kuwa, watu wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu miliki bunifu (Intellectual Property) na namna wanavyoweza kunufaika.

"Wamiliki wa mazao ya akili (Intellectual Property) ndio mabilionea wa sasa, mfano mzuri ni Mfanyabiashara wa Marekani Ellon Musk. Vyuo Vikuu vinapaswa kujikita kwenye tafiti ambazo zitapelekea kupata hataza za kutosha, kama njia ya kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii", amesema Afisa Sheria kutoka BRELA Wakili Calvin Rwambogo.

Vyuo vinapaswa kuwa na ofisi maalum kwa ajili ya kusimamia bunifu na kuziendeleza, kwa kuhakikisha miliki bunifu zote zinapata hataza, kwa kuwa na timu ya masoko pamoja na kutafuta wawekezaji wa hataza hizo. Pia, kabla ya kupeleka kazi za bunifu kwenye maonesho (exhibition), ni vyema wakahakikisha wamepata hataza kutoka BRELA, ameongeza wakili Rwambogo.

Semina hii ambayo itadumu kwa muda wa siku tatu (3), ina lengo la kutoa elimu kuhusuh huduma zinazotolewa na BRELA, usajili wa hataza pamoja na alama za biashara na huduma.

Comments
Send a Comment