MITI 6,500 YAPANDWA KAMPENI YA KUKIJANISHA UDOM
Chuo kikuu cha Dodoma kimepanda miti 6,500 ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni ya Kukijanisha Chuo Kikuu cha Dodoma ambayo ilihusisha upandaji wa miti katika maeneo ya mpaka wa UDOM.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo ambalo limefanyika tarehe 14 Desemba 2024 Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina amesema ni mwendelezo wa Kampeni ya Kukijanisha UDOM kuhakikisha kila mwaka inapadwa miti ya kutosha ili kulinda mazingira yetu na kufanya UDOM mahali pa kuvutia.
"UDOM tuna eneo kubwa sana na lazima tuhakishe kuwa tunapanda miti ya kutosha na leo tumeanza kupanda mipaka yote inayozunguka Chuo kuhakisha kuwa tunatunza mazingira na kulinda mipaka yetu na zaidi kupendezesha eneo letu, hatujamaliza mipaka yote hii ni awamu ya kwanza tutaendelea tena maeneo mengine yote " Alisisitiza.
Kaimu Rasi Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati Prof. Jefta Sunzu amesema miti iliyopandwa ni 6,500 kwa umbali zaidi ya Kilomita 20 pia amesitizia kuwa miti iliyopandwa italindwa na kutunzwa.
Naye Makamu wa Rais Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dodoma ( UDOSO) Bi. Jackline Humbaro amewapongeza Wanafunzi kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo na ameahidi kwa niaba ya wanafunzi kuwa wanafunzi wataendelea kushiriki kikamilifu katika Kampeni hii.
Katika Kampeni hii, miti takribani 20,000 itapandwa katika mpaka wa Chuo Kikuu cha Dodoma.