UDOM YAZINDUA KONGAMANO LA KWANZA LA KISAYANSI LA AFYA


  • 2 weeks
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kupitia Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii na Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa, kimezindua Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Afya “The first UDOM Scientific Conference on Health (USCHe)” lenye kauli mbiu Afya na Ustawi kwa Wote linalofanyika katika ukumbi wa Jiji la Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba kuanzia tarehe 29 hadi 31 Mei 2024.

 
Lengo la kongamano hilo ni kubadilishana ujuzi na uzoefu katika masuala ya Afya na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutekeleza lengo la 3 la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa (SDG3) lililopitishwa mwaka 2015 lenye lengo la kuhakikisha maisha yenye Afya kwa Ustawi kwa Wote kufikia mwaka 2030.
 
Akizungumza katika uzinduzi wa Kongamano hilo Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin O. Mollel, amesema Serikali inashirikiana kwa karibu na wadau vikiwemo Vyuo Vikuu kufanya tafiti ambazo zinasaidia kuleta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya Kitanzania. Mhe. Mollel alieleza kuwa Wizara ya Afya itashirikiana na UDOM katika kuhakikisha kongamano hili linafanyika kila mwaka na kwa mafanikio makubwa.
 
“Wizara inatambua kazi nzuri inayofanywa na Chuo Kikuu cha Dodoma, Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya na niwahimize kuendelea kuwekeza katika kufanya utafiti; “Wizara ya Afya tutashirikiana na nyie kwa karibu katika kuhakikisha kongamano hili linafanyika kila mwaka na kwa mafanikio makubwa zaidi.” Alisisitiza 
 
Kwa Upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka aliishukuru Serikali kwa kusogeza huduma Bora za Afya kwa Watanzania wote. Alieleza kuwa, kutokana na ushirikiano anaoupata kutoka serikalini, Chuo Kikuu cha Dodoma kimeweza kufanikisha majukumu yake ya kutoa huduma kwa jamii na ufundishaji kwa kushirikiana na Hospitali za Dodoma na mikoa ya jirani. Alieleza pia kuwa, ushirikiano huu umewezesha kufanyika upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 40 ambapo imepunguza gharama za wagonjwa hawa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
 
“UDOM ni mali ya Watanzania na tupo kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania; kwa muda mrefu tumekuwa tukishirikiana na Hospitali mbalimbali hasa za mkoa wa Dodoma katika kutoa elimu na huduma za afya kwa jamii. Nichukue fursa hii kuzishukuru Hospitali zote tunazoshirikiana nazo na kwa namna ya pekee Hospitali ya Benjamini Mkapa ambayo tunashirikiana katika kutoa huduma ya upandikizaji figo.” Aliongeza Prof. Kusiluka.
 
Kongamano hilo lilihudhuuwa na wageni kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania, Japan, Uingereza, na India.
Comments
Send a Comment