UDOM YAANZA UJENZI WA MABWENI IRINGA
Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza ujenzi wa Mabweni wenye thamani ya Bilion 3.4 kwa ajili ya Wanafunzi wanaofanya Mafunzo ya Vitendo ya Udaktari Mkoani Iringa.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika eneo hilo la ujenzi tarehe 13 Mei 2025 Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka amesema lengo kubwa la Kujenga eneo hilo ni kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira mazuri kwa ajili ya kujifunza na alisisitiza kuwa hata wanafunzi wengine ambao sio kada ya Afya wanapokuja Iringa au maeneo jirani kufanya mafunzo kwa vitendo wanaweza wakatumia mabweni hayo.
Naye; Mkurugenzi wa Milki na Majengo Chuo Kikuu cha Dodoma Injinia Stella Kyabula amesema, Mkandarasi wa Mradi huo ni Kampuni ya KGG Investment kutoka Jijini Dar es Salaam ambapo amepewa muda wa miezi 18 mradi ukamilike ambapo kwa mujibu wa Mkatata atatakiwa Kukabidhi majengo tarehe 13 Mei 2026.
“ Jengo hili likikamilika litaweza kuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 240, kwa mara moja, na bado tunaeneo la kutosha kuanzisha miradi mingine yenye tija kwa Taasisi” alisisitiza
Kwa upande wake; Mhandisi wa Eneo hilo la Ujenzi Injinia Hamis Rhumba, amesema mpaka sasa wamefikia zaidi ya asilimia 10% ya utekelezaji mradi na kuishukuru Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu wa ujenzi unaoendelea.