UDOM NA IPA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANAFUNZI WA SHAHADA ZA UZAMILI


  • 16 hours
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA), wamefanya kikao cha majadiliano kuhusu maendeleo ya wanafunzi wa Shahada za Uzamili, ili kubainisha changamoto pamoja na njia za kuzitatua.

Kikao hicho kilifanyika Machi 12, 2025 katika Ukumbi wa Baraza (UDOM) na kuongozwa Mwenyekiti pamoja na Wajumbe kutoka pande zote mbili.

Akifungua kikao hicho, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka amesema, wasimamizi wa wanafunzi Shahada za Uzamili wanatakiwa kuwapa wanafunzi muda wa kuandaa tafiti zao vizuri.

“Tunajua zipo changamoto za kusoma wakati unafanya kazi, lakini kuna wakati huwa tunalazimika kutoa muda wa kutosha kwa wanafunzi wa Shahada za Uzamili kufanya tafiti nzuri ambazo zitasomwa mpaka kimataifa," aliongeza Prof. Kusiluka.

Prof. Kusiluka amewataka pia wajumbe wa baraza kupokea maoni, mapendekezo na ushauri, ili kusaidia mradi huu wa kwanza kuweza kukamilika na kufikia malengo.

Naye, Rasi wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) Dkt. Shaban Suleiman, amewataka wasimamizi wa wanafunzi kuwasimamia kwa haki ili waweze kumaliza kwa wakati.

”Tutafurahi kama wanafunzi hawa watamaliza kwa awamu na katunukiwa vyeti vyao," aliongeza Dkt. Suleiman.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar (IPA) Prof. Mwalimu Mmunga Mjengo amesema, tunataka wanafunzi wenye ujuzi walioandaliwa vizuri, kwa ajili ya kusaidia serikali yetu na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi (UDOM) Prof. Razack Lokina amesema, ipo haja ya kuboresha usimamizi kwa njia ya mtandao na ushauri elekezi, ili kuwapunguzia wanafunzi gharama. Pia ametaka kuwe na mazungumzo ya mara kwa mara kati ya wasimamizi wa wanafunzi.

Comments
Send a Comment