UDOM YAADHIMISHA SIKU YA FIGO DUNIANI
Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kupitia hospitali yake iliyopo Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii (CHSS), tarehe 13 Machi, 2025 imeadhimisha Siku ya Figo Duniani kwa kutoa huduma za matibabu pamoja na elimu bure kwa wananchi, kuhusu umuhimu wa kutunza figo ili kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa huo.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Nyerere Square na kuhudhuriwa na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Afya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, wataalamu wa afya kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma waliokuja kupata huduma hiyo.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Caroline Damian amesema, kwa nchi kama Tanzania takribani wagonjwa 4300 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotokana na figo, huku hali hiyo ikichangiwa na kukosekana kwa gharama za matibabu pamoja na elimu ya uelewa na amekipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa juhudi za kuokoa maisha kwa kutoa elimu na matibabu bure.
“Kampeni hii imeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma na ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kulinda figo na kuepuka gharama, kwa kuwapatia wananchi matibabu bure,” alisisitiza Dkt. Caroline.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha na Utawala (UDOM) Prof. Pendo Kasoga amesema, Chuo Kikuu cha Dodoma kimekuwa mdau mkubwa kwa kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo figo pamoja na huduma ya kusafisha Damu (Dialysis) kwa wagonjwa wa figo.
Naye, Mganga Mfawidhi kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Alfred Meremo amesema mpaka kufikia siku ya pili ya kampeni hiyo, tayari wamefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 500 na matarajio yao ni kuwafikia wananchi zaidi ya 1500.
Kila mwaka, Chuo Kikuu cha Dodoma hufanya maadimisho ya Siku ya Figo Duniani, ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ni, 'Gundua Mapema, Linda Afya ya Figo.'