BENKI YA DUNIA YAZITAKA TAASISI ZINAZOTEKELEZA MRADI WA HEET KUONGEZA KASI KATIKA UJENZI WA MIUNDOMBINU
Benki ya Dunia (WB), imetoa wito kwa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu Tanzania zinazotekeleza Mradi wa Elimu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kuongeza kasi katik eneo la ujenzi wa miundombinu na usimamizi, kutokana na kasi ndogo katika ujenzi wa Miundombinu inayoonekana kwa vyuo vingi kwa sasa.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi tarehe 03 Aprili 2025, siku ya pili ya kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu nchini, zinazotekeleza Mradi wa HEET na Benki ya Dunia, kinachoendelea katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akichangia kwenye uwasilishaji wa moja ya taarifa za maendeleo ya Mradi; Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bw. Nkahiga Kaboko, amesema ni vizuri vyuo vikaongeza umakini katika kuwasimamia wakandarasi ili kumaliza kwa wakati shuguli za ujenzi kama yalivyo malengo ya mradi, badala ya kutegemea muda wa mradi kuongezwa.
Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Peter Msofe, ametilia msisitizo suala hilo na kutoa msimamo wa Wizara kuendelea kufuatia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo akiwataka wahusika wote wa Mradi kuhakikisha usimamizi wa kutosha unafanyika, ili wakandarasi waweze kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa mikataba.
“Jitahidini kuongeza usimamizi na umakini kwa wakandarasi ili wamalize kazi kwa muda uliokubalika, kasi ya ujenzi kwa vyuo vingi bado hairidhishi na muda tuliobaki nao kufika Juni 2026, ni mdogo” alisisitiza
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mratibu Msaidizi wa Mradi, Dkt. Happiness Nnko; amesema kwa upande wa Miradi ya Ujenzi, Chuo kinaendelea na Ujenzi wa Madarasa Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi CoESE, ambao umekamilika kwa asilimia 24.8, ujenzi wa Maabara Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati (CNMS) asilimia 9%, wakati ujenzi wa Kampasi mpya Njombe bado haujaanza; kutokana na taratibu za manunuzi za kumpata Mkandarasi wa Ujenzi kutokamilika.
Amesema changamoto kubwa katika ujenzi wa miundombinu zinatokana na mlolongo mrefu wa kuwapata wakandarasi wenye sifa huku baadhi ya wakandarasi kukosa vibali na hivyo kuchangia kwa sehemu kubwa ujenzi kuchekewa kuanza.
“Miradi yote hii imepangwa kukamilika mapema mwaka 2026, na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma, imejipanga kuhakikisha Miradi yote inakamilika kwa wakati uliopangwa pamoja na changamoto zilizopo” Alisisitiza Dkt. Nnko.
Aidha; ameyataja maeneo mengine ambayo UDOM imefanya vizuri kuwa ni pamoja na kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) ambapo hadi kufikia kipindi cha taarifa hii, Chuo kimefanikiwa kwa asilimia 84.9% ya malengo, ambapo kati ya wanafunzi 44,567 waliokusudiwa kufikiwa nchi nzima, UDOM imewafikia wanafunzi 34,241; kati ya hao wanawake ni asilimia 32.3% na wanafunzi wenye mahitaji maalumu 214.
Kwa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mradi wa HEET unatekelezwa kwa tengeo la bajeti la jumla ya Dola za Kimarekani 23,000 na miradi yote inatazamiwa kukamilika mwezi Juni 2026.