WANATAALUMA WANOLEWA UANDISHI WA TAFITI


  • 20 hours
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Chama cha Wanataaluma cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA), kimeandaa warsha maalumu ya siku 2 yenye lengo la kutoa mafunzo ya matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) pamoja na mbinu za Uhakiki wa Kitaaluma (Systematic Review) kwa wanataaluma wa UDOM.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea katika Ukumbi wa Maktaba ya Kompyuta uliopo Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu (CIVE), leo tarehe 22 Aprili 2025, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, amepongeza juhudi za UDOMASA katika kuwawezesha washiriki kuendana na mabadiliko ya Kiteknolojia na mahitaji ya kisasa ya utafiti.

"Katika mazingira ya sasa ya kitaaluma, matumizi ya Akili Mnemba ( AI) si chaguo tena bali ni hitaji. Tunahitaji kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia hizi kwa ufanisi ili kuongeza ushindani wetu katika utafiti na machapisho." Aliongeza Prof. Lokina.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDOMASA, Dkt. Gerald Shija, ameeleza kuwa warsha hiyo ni sehemu ya mkakati wa chama hicho katika kuinua kiwango cha Taaluma miongoni mwa wanachama wake, sambamba na kuongeza mchango wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika jamii kupitia tafiti bora na zenye tija.

"Ni matarajio yetu kuwa washiriki watatumia maarifa haya si tu kwa manufaa yao binafsi, bali pia kusaidia wenzao na wanafunzi katika kuimarisha mazoea ya uandishi wa kitaaluma unaozingatia ushahidi," aliongeza Dkt. Shija.

Washiriki wa warsha hiyo wanatarajiwa kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo namna ya kutumia majukwaa mbalimbali ya Akili Mnemba katika kutafuta maarifa, kuchanganua matokeo ya tafiti, kuandika Machapisho, na kufanya uhakiki wa kina wa maandiko ya kitaaluma kwa kutumia mbinu sahihi na za kisasa.

Comments
Send a Comment