UDOM YAWANOA WANAFUNZI WA SHAHADA ZA UZAMIVU
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Kurugenzi ya Shahada za Uzamili, wameandaa mafunzo ya wiki moja kuanzia Disemba 16 hadi 20, 2024, yenye lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika uandishi wa Pendekezo la Utafiti (Research Proposal).
Akifungua Mafunzo hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, amewapongeza wanafunzi hao kwa kuchagua kujiunga na UDOM na kuwataka kuzungatia mafunzo hayo yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuandika mapendekezo ya utafiti.
Amewaasa kutokuwa waoga wanapokosolewa na wasimamizi wao kwani lengo la pamoja ni kuandika kazi zenye ubora na tija kwa jamii.
“ Tumieni muda huu vizuri kujifunza mambo mapya, na kusoma tasnifu za waliowatangulia ili kupata mawazo mapya na kuandika tasnifu zenye ubora “ alisisitiza
Amewataka kutumia teknolojia vizuri, ikiwemo Akili Mnemba (Artificial Intelligence) iwasaidie kupata mawazo mapya na sio kuiachia kuitumia kufanya udanganyifu.
Ameahidi ofisi yake kuendelea kuandaa mafunzo ya aina hiyo kila inapohitajika ili kuwawezesha kila mmoja kumaliza ndani ya muda, kwakuwa ndiyo malengo ya Chuo ya kila mwanafunzi kumaliza kwa wakati.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Shahada za Juu (UDOM) Dkt. Julius Ntwenya, amesema, wanafunzi wakizingatia mafunzo haya yanayotolewa, wataweza kumaliza elimu ya Shahada ya Uzamivu (PhD) kwa wakati uliopangwa na kwa ufaulu wa kiwango cha juu zaidi.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo , Bw. John Joseph Sichilima amepongeza juhudi za Chuo za kuandaa mafunzo hayo na kwamba yatawasaidia kuweza kuandika kwa usahihi Tasnifu na kwa wakati, na hatimaye kuhitimu kwa wakati.