UDOM YATOA MAFUNZO YA UANDISHI WA TAFITI KWA WANAFUNZI WA SHAHADA YA UZAMIVU
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeanza kutoa mafunzo ya siku 5 ya Uandishi katika Tafiti kwa wanafunzi wanaosoma shahada ya uzamivu (PhD).
Mafunzo haya yamejikita katika kuwawezesha watafiti kufanya tafiti zenye viwango na kuchapisha kazi zao katika viwango vya kimataifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kurugenzi ya Huduma za Maktaba pamoja na Kurugenzi ya Shahada za Juu, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Tafiti na Ushauri, Prof. Razack Lokina ameeleza kuwa mafunzo hayo yanafanyika ukiwa ni utaratibu ambao UDOM imejiwekea ili kuwajengea uwezo wanafunzi wa shahada ya Uzamivu kuandika tafiti zenye ubora wa kimataifa.
“Matarajio yetu ni kuwa baada ya mafunzo haya mtajengewa uwezo katika kutafuta, kupata na kutathmini machapisho ya kitaaluma pamoja na kutumia teknolojia katika kufanya marejeo bila kuvunja sheria za kiuandishi”. Alisisitiza Prof. Lokina
Naye: Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba UDOM, Dkt. Grace Msoffe, amesema kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanafunzi katika kufanya marejeo, kutumia teknolojia kwa ajili ya kuhifadhi taarifa, matumizi ya akili mnemba kwa kuzingatia sheria kupitia miongozo na mifumo mbalimbali yenye kanzi data za Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mmoja ya wanafunzi waliohudhuria Mafunzo hayo, Bi. Jenifer Cosmas kutoka Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati CNMS amesema;
Mafunzo hayo yatakuwa na msaada sana kwani yatamuongezea ujuzi wa kutumia teknolojia kwa ajili ya kuhifadhi taarifa pamoja na matumizi ya akili mnemba kwa usahihi.
Mafunzo hayo yamekuwa yakifanyika mara moja kila mwaka na yanawalenga wanafunzi wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu wa Shahada ya Uzamivu ili kuwajengea uwezo katika kukusanya, kuhifadhi pamoja na kutumia teknolojia katika kuandika tafiti zenye ubora.