UDOM YAZINDUA RASMI MRADI WA STEP-STUDY
huo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Graz cha nchini Austria na Chuo cha Ufundi Arusha, leo tarehe 23 Julai, 2025 wamezindua rasmi mradi wa (Step-Study) wenye lengo la kuboresha mafunzo ya Taaluma ya Ualimu kwenye Shule za Msingi na Vyuo ya Ualimu hapa nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo (UDOM) Prof. Lughano Kusiluka amesema, serikali imewekeza sana kwenye elimu, hivyo mradi mkubwa wa elimu kama huu utasaidia kwenye uboreshaji na uandaaji wa sera mbalimbali za elimu hapa nchini. Pia, alisisitiza kuhusu umuhimu wa vyuo vikuu kufanya tafiti mbalimbali na uvumbuzi.
" Kuwaandaa walimu wenye ubora, watakaowahamasisha wanafunzi kuwaza mema kwa ajili ya nchi yao, dunia na kuweza kujiandaa wao binafsi, ni somo la muhimu," alisisitiza Prof. Kusiluka.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Graz nchini Austria Prof. Heike Wendt amesema, mradi huu utasaidia kuhakikisha walimu wanaandaliwa vyema, ili waweze kuwafundisha wanafunzi vizuri. Amesema mradi huu pia utasaidia katika kutathmini kama nadharia zinazotumika sasa katika ufundishaji hapa nchini, zitatusaidia miaka ya mbeleni.
Aidha, Kiongozi wa Mradi huu ambaye pia ni Kaimu Rasi wa Ndaki ya Elimu (UDOM) Dkt. Abdallah Seni amesema, mradi huu utasaidia katika kuboresha mitaala pamoja na kuwapatia walimu ujuzi unaoendana na karne hii ya 21.
Naye, Naibu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Dkt. Yusuph Muhando amesema, mradi huu utasaidia kuimarisha elimu ya msingi hapa nchini, pamoja na kuimarisha mahusiano ya kitaifa na kimataifa kupitia tafiti watakazozifanya kwa pamoja.
Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Musa Malalika amesema, wizara ipo tayari kutoa ushirikiano ambao utasaidia katika kupata taarifa zitakazoboresha mfumo wa elimu hapa nchini.
Pia, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Sylivester Balige amesema, wao kama wadau wakuu wako tayari kutoa ushirikiano katika kufanikisha mradi huu, kwani wanazifahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu wa Shule za Msingi hapa nchini.